SwahiliHub on Sept 12, 2015

WASICHANA WAWAZIDI MAARIFA WAVULANA SHINDANO LA INSHA

DnE-Kitabu Will

Mwanzilishi na Afisa Mkuu Mtendaji wa E-Kitabu Bw Will Clurman akizungumza wakati wa hafla ya staftahi Septemba 11, 2015 ambapo washindi wa Insha za kidijitali walibainika. Picha/JEFF ANGOTE

Na LEONARD ONYANGO

Imepakiwa – Friday, September 11   2015 at  12:06

Kwa Mukhtasari

Wasichana wamebwaga wavulana katika shindano la uandishi wa insha za kidijitali la 2015 linalofadhiliwa na kampuni ya kusambaza vitabu kupitia mfumo wa kidijitali, eKitabu kwa ushirikiano na Wizara ya Elimu na wadau wengineo.

 

WASICHANA wamebwaga wavulana katika shindano la uandishi wa insha za kidijitali la 2015 linalofadhiliwa na kampuni ya kusambaza vitabu kupitia mfumo wa kidijitali, eKitabu kwa ushirikiano na Wizara ya Elimu na wadau wengineo.

Kulingana na matokeo yaliyotangazwa Ijumaa, wasichana kote nchini wametwaa nafasi za kwanza na pili katika vitengo vyote vya shule za msingi na sekondari.

Msichana kutoka shule ya Loreto Convent Valley Road, Nairobi ndiye mwandishi bora wa insha ya Kiswahili katika kitengo cha shule za msingi baada ya kuibuka na alama 80.63 huku mwenzake wa Hill School Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu akitawazwa mshindi kwa alama 82.2 katika kitengo cha shule za upili.

Wasichana kutoka shule ya msingi ya Kericho na ile ya Tetu Girls ya Kaunti ya Nyeri waliibuka katika nafasi ya pili na tatu baada ya kupata alama 79.3 na 76.8 mtawalia katika uandishi wa insha ya Kiswahili kitengo cha shule za msingi.

Msichana kutoka shule ya sekondari ya Moi Girls, Kaunti ya Uasin Gishu aliibuka wa pili kwa alama 80.8 huku mvulana kutoka shule ya upili ya Malindi, Kilifi akishikilia nafasi ya tatu kwa alama 79.8 katika kitengo cha uandishi wa insha ya Kiswahili.

Katika kitengo cha uandishi wa insha ya Kiingereza, msichana wa shule ya Little Angels, kaunti ya Isiolo alitawazwa mshindi kwa alama 86.9 katika kitengo cha shule za msingi. Mwanafunzi kutoka shule ya Thika Road Christian, Nairobi aliibuka nafasi ya pili kwa alama 84 huku wenzake wa wawili kutoka shule ya msingi ya Mbagathi Road wakiibuka katika nafasi ya tatu na nne kwa alama 82.7 na 82.2 mtawalia.

Insha ya Kiingereza

Katika kitengo cha shule za upili, wanafunzi wa shule za Moi Girls -Eldoret,  Precious Blood Riruta- Nairobi na Maranda, Siaya walitangazwa waandishi bora wa insha ya Kiingereza baada ya kupata alama 87, 85 na 83 mtawalia.

“Kampuni ya eKitabu imekuwa ikiandaa shindano la uandishi wa insha kila mwaka tangu 2013. Mwaka huu tulipokea jumla ya insha 2,100 kutoka kwa wanafunzi wa zaidi ya shule 400 za kaunti 45. Hatukufanikiwa kupata insha kutoka Kaunti za Wajir na Pokot Magharibi,” akasema Will Clurman, Mkurugenzi Mkuu wa eKitabu.

“Katika insha ya mwaka huu wanafunzi walitakiwa kuandika barua kwa Rais wa taifa la Kenya wakimweleza kuhusu maisha yao kama wanafunzi wa kidijitali chini ya kichwa : ‘Kwa Rais Mpendwa….maisha yangu kama mwanafunzi wa kidijitali’,” akaongezea. Gazeti la Taifa Leo na tovuti ya Swahilihub wamefadhilia tuzo za vipakatalishi 6 vitakavyotunukiwa washindi watatu bora katika kitengo cha shule za msingi na za upili. Wafadhili wengine ni kama kampuni za HP, MTN, Samsung miongoni mwa wengine.Washindi watatuzwa vifaa vilivyo na vitabu vya kidijitali, fedha za kufadhili masomo yao na hata walimu na shule zao kutambuliwa,” akasema Bw Clurman.

Washindi yatatangazwa rasmi mnamo Septemba 23 wakati wa Maonyesho 18 ya Kimataifa ya Vitabu ya Nairobi katika ukumbi wa Sarit Centre, Nairobi.

“Insha bora zitakabidhiwa kwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia, Fred Matiang’i ambaye baadaye ataziwasilisha kwa Rais Uhuru Kenyatta.

Original article:  http://www.swahilihub.com/habari/HABARI-ZA-MIKOANI/wasichana-mabingwa-shindano-la-insha/-/1333058/2866526/-/64lifc/-/index.html

eKitabu is East Africa’s premier ebook store. We distribute ebooks and interactive content. Search for ebooks of your choice from www.ekitabu.com . Pay by Mpesa or credit card and read with the free eKitabu App on android smartphone, tablet, laptop or PC.

%d bloggers like this: