Swahili Hub Sept 25th, 2014

WASHINDI WA KWANZA WA UANDISHI WA INSHA KIDIJITALI WATUZWA

Mshindi wa e-Kitabu

Afisa Mkuu Mtendaji wa e-Kitabu Bw Will Klurman akitoa Zawadi ya hundi ya laki moja kwa mshindi wa insha Septemba 25, 2014. Picha/HUGHOLIN KIMARO

Na HUGHOLIN KIMARO

Imepakiwa – Thursday, September 25   2014 at  09:11

Kwa Mukhtasari

Washindi wa uandishi wa insha bora kwa njia ya kieletroniki kutoka katika kaunti zote 47 walituzwa Jumatano katika maonyesho ya vitabu yanayoendelea katika jumba la Sarit Centre, Westlands, Nairobi.

 

MAONYESHO ya 17 ya Vitabu ya Kimataifa jijini Nairobi mwaka huu wa 2014 yalianza katika ukumbi wa Sarit Centre kwa hafla isiyokuwa ya kawaida.

Katika ukumbi huo, kulikuwa na hafla ya kuwatuza washindi wa insha bora za kidijitali kutoka kaunti zote 47 nchini walioshiriki katika shindano hili ambalo limeandaliwa humu nchini kwa mwaka wa pili sasa. Walimu, wanafunzi na wadau tofauti katika nyanja za elimu walihudhuria kikao hicho.

Shindano hili la insha za kidijitali kwa wanafunzi wa shule za Sekondari na wale wa viwango vya juu vya shule za Msingi yanaandaliwa na Kampuni ya E-Kitabu ambayo hutoa huduma za kusambaza vitabu vya kielektroniki au kidijitali na huduma nyingine za kikompyuta.

Akizungumza na wanahabari wa Swahilihub katika ukumbi wa Sarit mtaani Westlands, jijini Nairobi, Afisa Mkuu Mtendaji wa e-Kitabu Bw Will Klurman alisema kuwa kauli mbio ya  kampuni hiyo ‘Tunaenda Digital’ imejidhihirisha kwa ufanisi mkubwa wa kupata washiriki 2,062 katika insha hizo za Kingereza na chache za Kiswahili.

Mashindano hayo yaliandaliwa kwa ushirikiano wa Kampuni ya eKitabu na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Bw Klurman alisema kuwa juhudi za mradi wa eKitabu wa kufanikisha matumizi ya mtandao kuboresha mfumo wetu wa elimu ulialika zaidi ya shule 2,000 za serikali na za kibinafsi kote nchini kuleta insha zao kwa njia ya mtandao kwa katika anwani http://www.essay.kitabu.com.

Uandishi huu ulianza Aprili hadi Agosti kwa wanafunzi wa vitengo viwili; madarasa ya juu katika shule za msingi yaani darasa la 5 hadi la 8 na wanafunzi wote wa sekondari.

Mada ya insha ilikuwa: Teknolojia katika Elimu Yangu: Ndoto au Uhalisia? Shindano lenyewe lilivutia washiriki kutoka katika shule 271 wa kaunti zote 47.Insha zenyewe zilitoka kwa wanafunzi wa shule za mijini na wengine wa shule mashambani kama West Pokot, Migori, Turkana na Mandera.

Kilicho washangaza washiriki katika hafla hiyo ni kuwa kulikuwa na ongezeko la 319% kwa walioshiriki ikilinganishwa na mwaka jana sawia na ongezeko la 287% katika shule zilizoshiriki ikilinganishwa na mwaka 2013.

Washindi wa shule za Msingi ambao ni sita bora walikuwa Vanessa Ndirangu wa Thika Road Christian School,  Sasqia Kerubo wa Lavington Primary,  Rhodah Agola wa Kwa Njenga Primary School, Juliet Atieno, Drive In Primary, Bright Langat wa  Flourspar Primary School na Caleb Loisula kutoka Maralal Primary School.

Washindi watano bora katika kitengo cha sekondari walikuwa Emmanuel Kansio kutoka Starehe Boys’ Center, Susan Wariara kutoka Starehe Girls Center, Tito Yak kutoka Alliance High School, Hope Chemutai kutoka  The Kenya High School, Roseline Okemwa kutoka Asumbi Girls High School

Wadhamini wakuu wa mashindano haya walikuwa Wizara ya Elimu, Kampuni za HP, Mustek East Africa, MTN Kenya, Oxford University Press, Longhorn Publishers na Elimu. Zawadi zilizotolewa kwa washindi ni pamoja na udhamini wa masomo washindi watatu wa kwanza katika vitengo vyote. Mshindi wa kwanza katika kila kitengo alijinyakulia kipakatalishi. Waamuzi walikuwa na zawadi ya pekee kwa washindi wa vitengo vyote katika Uchoraji wa kisanaa na Kiswahili.

Matokeo haya yalitangazwa wakati mahakama kuu inatoa uamuzi wa kufutilia mbali tenda/zabuni za kutoa na kusambaza vipakatalishi kwa wanafunzi wote wa darasa la kwanza nchini kufuatia ahadi iliyowekwa na Chama wa Jubilee wakati wa kampeni za siasa wakati wa uchaguzi uliopita.

Mtalaa

Akiongea katika maonyesho hayo ya vitabu ya kila mwaka, Bw John Temba, Mkuu wa Masuala ya Tarakilishi katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia aliongeza kwamba mtalaa wa kompyuta kwa darasa la kwanza u tayari lakini kikwazo kimekuwa kesi iliyokuwa mahakamani. Alipokuwa akizungumza kesi hii ilikuwa Inaendelea na uamuzi huu wa kufutilia mbali tenda hizo haukuwa umefikiwa bado.

“Watu wengi wanafikiria juu ya vipakatalishi tu bila kujua kwamba  hivi ni vifaa tu ambavyo vinahitaji kuandaliwa mambo ya kufunzwa. Sharti tujiweke tayari ili vipakatalishi vitakaposambazwa shuleni mitalaa yake iwe tayari na ianze kutumika mara moja,” akasema Bw Temba kauli iliyokaririwa kikamilifu na mwenyekiti wa Chama Cha Wachapishaji nchini (KPA) Bw Lawrence Njagi.

Bw Klurman alifurahishwa na mradi huu kwa kuwa Ndoto za Wakenya hata waliopembeni mbali na jiji kuu kama Mandera, Samburu, Homa Bay na Malindi waliweza kushiriki na hata kushinda.

Original Article: http://www.swahilihub.com/habari/MAKALA/-/1310220/2464516/-/15n6t59/-/index.html

eKitabu is East Africa’s premier ebook store. We distribute ebooks and interactive content. Search for ebooks of your choice from www.ekitabu.com . Pay by Mpesa or credit card and read with the free eKitabu App on android smartphone, tablet, laptop or PC.

%d bloggers like this: